Header Ads

DOTK-BAR

MAVUNDE AAGA UBUNGE KWA HESHIMA, AACHIA MFUMO WA KIDIGITALI KUPOKEA KERO ZA WANANCHI




NA DOTTO KWILASA, DODOMA

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ametangaza rasmi kuhitimisha safari yake ya miaka 10 ya kulitumikia jimbo hilo, huku akiweka historia kwa kuzindua mfumo wa kwanza wa kidigitali wa kupokea na kushughulikia kero za wananchi pamoja na kugawa simu janja kwa wenyeviti wa mitaa 222.

Hafla hiyo ya kihistoria imefanyika jana jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa mitaa, wataalamu wa TEHAMA, pamoja na wananchi mbalimbali waliofika kushuhudia kilele cha uongozi wake wa awamu mbili.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mavunde amesema anaondoka katika nafasi ya ubunge akiwa hana deni la kisiasa kwa wananchi waliompa dhamana ya uongozi kwa kipindi cha muongo mmoja.

“Leo ndiyo siku yangu ya mwisho kama Mbunge wa Dodoma Mjini nawashukuru kwa kuniamini na kunipa heshima ya kuwa kiongozi wenu kwa miaka kumi. Nimejitahidi kuishi kama mtumishi wa watu, siyo kiongozi wa majukwaa,” amesema

Katika kuimarisha uwajibikaji na kujenga msingi wa utumishi endelevu, Mavunde alizindua mfumo wa TEHAMA ambao utawawezesha wenyeviti wa mitaa kupokea taarifa za wananchi kwa wakati na kuzifikisha kwa viongozi husika kwa haraka na uwazi zaidi.

Amesema mfumo huo ambao ni wa kwanza kuanzishwa katika ngazi ya jimbo nchini utaunganishwa katika kata zote 41 za Dodoma Mjini na utaendelea kutumika hata baada ya yeye kuondoka madarakani.

“Tumeingia kwenye zama za utawala wa kidigitali,kupitia mfumo huu, taarifa ya mwananchi itamfikia kila kiongozi wa eneo husika hata kama mbunge au mwenyekiti hakupatikana kwa simu. Hakuna tena kero kupotea,” ameeleza.

Mavunde amesema kila mwenyekiti wa mtaa amekabidhiwa simu janja kama kifaa rasmi cha kazi na si anasa, akibainisha kuwa vifaa hivyo vimetengenezwa nchini katika kiwanda cha Mkuranga, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya viwanda na teknolojia ya ndani.

Aidha, ametoa rai kwa mbunge atakayechukua nafasi yake kuhakikisha anautumia na kuuendeleza mfumo huo ili kulinda ahadi kwa wananchi na kuendeleza utumishi wa kweli kwa jamii ya Dodoma Mjini.

“Nitahakikisha mbunge atakayekuja anaelewa mfumo huu. Sitaki historia ya utumishi wetu izimike. Nimejitoa bila kujibakiza na sitaki kuondoka nikiwa na deni kwa watu wangu,” alisema kwa msisitizo.

Katika kueleza chanzo cha msimamo wake wa kuwa kiongozi wa vitendo, Mavunde alisimulia tukio lililomgusa kwa undani alipomkuta mwananchi mmoja akiwa amebeba maiti juu ya pikipiki kwa ajili ya kuisafirisha kwenye mazingira magumu.

“Hilo tukio lilinigusa sana,nikasema, mimi ni mbunge, siwezi kulikalia kimya. Badala ya kutoa michango kila siku, niliamua kununua gari kwa ajili ya kusaidia shughuli za usafirishaji wa miili. Wapo waliotukana, lakini leo gari hilo linaendelea kuhudumia jamii,” ameeleza kwa hisia.

Katika hatua nyingine, Mavunde alitangaza kutoa mchango wa shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuanzisha SACCOs ya wenyeviti wa mitaa wa Dodoma Mjini, kwa lengo la kuwaimarisha kiuchumi na kuwapa nguvu zaidi ya kuhudumia wananchi.

“Tutabaki pamoja daima, tutatenganishwa na mipaka ya kijiografia tu lakini moyo wangu utaendelea kubaki na watu wa Dodoma Mjini,” ameeleza



No comments

Powered by Blogger.