Mwanza Yajipanga Kuwa Kitovu cha Madini Nchini: Wachimbaji Wadogo Wapewa Kipaumbele
Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Katika kuendeleza dira ya uchumi jumuishi unaotegemea rasilimali za ndani, Mkoa wa Mwanza umejielekeza rasmi kwenye kuimarisha sekta ya madini, ukilenga kuwa moja ya mikoa kinara wa uzalishaji wa madini kwa viwango vya kitaifa na kimataifa.
Akizungumza jijini Dodoma Mkuu wa Mkoa, wa Mwanza Said Mtanda, amesema kuwa mikakati ya Mkoa inalenga kuunganisha fursa za wachimbaji wadogo na wawekezaji wakubwa ili kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi wa kawaida, halmashauri na serikali kuu kwa ujumla.
“Tumeamua kuifanya sekta ya madini kuwa injini mpya ya uchumi wetu. Mwanza tuna madini ya kutosha, nguvu kazi ya vijana ipo, na serikali imejipanga kuhakikisha wachimbaji wanapata elimu, usajili, na maeneo rasmi ya kuchimba kwa usalama na heshima ya sheria,” amesema Mhe. Mtanda.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, maeneo kama Kasanda na Ishokela Hela, yaliyopo Wilaya ya Misungwi, yamekuwa yakionesha msukumo mkubwa wa shughuli za uchimbaji mdogo wa madini, hivyo serikali imechukua hatua za haraka kufanya utambuzi rasmi wa maeneo hayo, kuwaandikisha wachimbaji, na kuwapatia mafunzo ya kitaalam.
Amezungumzia Mpango Maalum wa Mkoa kwa Wachimbaji Wadogo kuwa Mkoa utahakikisha hakuna tena uchimbaji holela unaoweza kusababisha migogoro au uharibifu wa mazingira, Mkoa umezielekeza ofisi za Afisa Madini Mkazi kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa mitaa na kata ili kutoa elimu ya sheria, mazingira, usalama wa wachimbaji, na namna bora ya kutumia teknolojia nyepesi kwenye uchimbaji.
Aidha, amesisitiza wachimbaji wadogo kujifunza kuhusu ushirikiano wa vikundi na uwekezaji wa pamoja (cooperatives) ili waweze kukua na kuingia katika mfumo rasmi wa kibiashara wa madini.
Amesema Miongoni mwa matarajio makubwa ya sekta ya madini mkoani Mwanza ni uzinduzi wa Mgodi wa Kimataifa wa Nyanzaga, unaotarajiwa kuwa miongoni mwa migodi mikubwa ya dhahabu barani Afrika.
Mgodi huo unaotarajiwa kuanza kazi hivi karibuni, unatoa matumaini ya ajira kwa maelfu ya wakazi wa Mwanza, pamoja na kuongeza mapato kwa halmashauri husika kupitia ushuru, huduma za kijamii na fursa za biashara zinazouzunguka.
“Ujio wa Nyanzaga si tu unamaanisha ajira, bali pia unatuonesha kuwa Mwanza iko tayari kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya madini,” amesema Mtanda
Kwa mujibu wa tathmini ya Mkoa, mwelekeo huu wa kimkakati wa kuendeleza madini unakwenda sambamba na kauli mbiu ya kitaifa ya "Madini ni Utajiri", lakini Mwanza imeipa tafsiri ya kipekee — “Madini kwa maendeleo ya wote”.
Amesema Serikali inatarajia kuona ongezeko la mapato, kupungua kwa migogoro ya ardhi na usimamizi bora wa mazingira kadri wachimbaji wadogo wanavyoingia kwenye mfumo rasmi wa uchimbaji na biashara ya madini.




No comments