Header Ads

DOTK-BAR

SADC Yaitambua Tanzania Kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika




Na Dotto Kwilasa – Harare, Zimbabwe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametajwa kuwa kinara namba moja barani Afrika katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua iliyotambuliwa rasmi na Mawaziri wa Nishati na Maji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) waliokutana jijini Harare, Zimbabwe.

Taarifa hiyo imetolewa Julai 3, 2025, wakati wa mkutano wa SADC uliohudhuriwa na mawaziri na wataalam kutoka nchi nane wanachama, ambapo Tanzania imepongezwa kwa hatua kubwa ilizopiga katika kutekeleza ajenda ya kitaifa ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo uwekezaji wa kimkakati, uelimishaji na ubunifu wa matumizi mbadala wa nishati rafiki kwa mazingira.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga alisema kuwa Serikali ya Tanzania imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya nishati safi kwa kushirikiana na sekta binafsi, jamii na taasisi za kimataifa, kupitia mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024–2034.

Mhe. Kapinga alitoa wito kwa nchi wanachama wa SADC kuweka mikakati madhubuti ya pamoja na kuwa wabunifu katika kusukuma mbele agenda hiyo, huku akitoa mfano wa mafanikio ya Tanzania katika matumizi ya mkaa mbadala kama briquettes na majiko banifu ambayo yanapunguza utegemezi wa kuni na mkaa wa kawaida.

Amesisitiza kuwa uelimishaji wa jamii kuhusu madhara ya matumizi ya nishati chafu ni jambo la msingi ambalo linapaswa kupewa msukumo mkubwa ndani ya jumuiya, kwa kuwa na kampeni za pamoja zenye ujumbe wa kuhamasisha tabia mpya ya matumizi ya nishati salama na endelevu.

Katika hatua nyingine, wanachama wa SADC walitoa pongezi kwa Tanzania kwa kufanikisha kwa mafanikio makubwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Nishati Afrika (Misheni 300 – M300) uliofanyika jijini Dar es Salaam, wakisema mkutano huo umeweka Tanzania katika ramani ya kimataifa ya mageuzi ya nishati.

Waziri wa Nishati wa Malawi, Mhe. Ibrahim Matola alimtaja Rais Samia kama kiongozi mwenye maono makubwa, akisema Tanzania inapaswa kuwa balozi wa nishati safi ya kupikia kwa nchi wanachama wa SADC kutokana na hatua inazochukua kuunganisha sera, elimu na uwekezaji kwa pamoja.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Suzan Kaganda pamoja na wakuu wa taasisi za Nishati kutoka Tanzania wakiwemo REA, TANESCO, TPDC na EWURA, wakiongozwa na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme, Mha. Styden Rwebangila.







No comments

Powered by Blogger.