Header Ads

DOTK-BAR

Wananchi Wafaidi Matunda ya Serikali Tabora: Umeme, Maji, Afya Boresha Maisha Kwa Kasi Mpya




Na Husna Zakayo,Dodoma

Mwananchi wa Tabora sasa wanajivunia kupata huduma bora karibu na makazi yao ikiwemo  huduma za afya, elimu, maji, umeme na barabara zimeimarika kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni.

Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mkoa wa Tabora umetumia zaidi ya Shilingi trilioni 15 kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020–2025.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Matiko Chacha, amesema kuwa miradi hiyo imesaidia kubadilisha maisha ya wananchi moja kwa moja. “Kila mwananchi sasa anaguswa. Mwanafunzi hasafiri umbali mrefu kwenda shule, mama mjamzito hapati tabu hospitali, na mkulima anaweza kutumia umeme kwa uzalishaji,” ameeleza.

Katika sekta ya afya, vituo vipya vya afya 30 vimejengwa, zahanati 109 zimekamilishwa, hospitali tano mpya zimefunguliwa na huduma za dharura kwa wajawazito zimeongezwa mara tatu. Hali hiyo imepunguza vifo vya kina mama na watoto wachanga.

Sekta ya maji imepata msukumo mkubwa pia, ambapo wananchi wa mijini na vijijini wameunganishwa na huduma safi na salama. Vijiji vilivyo na huduma ya maji vimeongezeka kutoka 393 hadi 505.

Umeme umeunganishwa kwenye vijiji vyote 722 vya mkoa, ikiwa ni hatua kubwa ya kupunguza giza, kuongeza fursa za ajira, biashara na elimu kupitia teknolojia.

Kwa upande wa elimu, shule mpya zimeongezeka, madarasa yameongezwa, na walimu zaidi ya 1,600 wameajiriwa. Ufaulu wa mitihani ya kitaifa umepanda, huku wanafunzi wengi wakifaulu kwa viwango vya juu katika darasa la saba, kidato cha nne na sita.




Wananchi pia wamewezeshwa kiuchumi kwa kupatiwa mikopo ya vikundi, msaada wa kilimo cha kisasa, skimu za umwagiliaji na ujenzi wa viwanda vidogo. “Mabadiliko haya yamewapa wananchi matumaini mapya ya kesho iliyo bora zaidi,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.


No comments

Powered by Blogger.