CHUO KIKUU HURIA NA JESHI LA POLISI RUVUMA WATOA MSAADA KITUO CHA WATOTO YATIMA CHIPOLE
Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Kituo cha kulelea watoto yatima na wenye mahitaji cha Chipole kilichopo Kata ya Magagura Halmashauri ya Songea Vijijini Mkoani Ruvuma kimepokea fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni moja na laki mbili (1,200,000) na mahitaji mbalimbali ikiwemo vyakula, nguo, na bidhaa nyingine zilizotolewa na jumuiya ya Chuo Kikuu Kikuu Huria cha Tanzania ikijumuisha wafanyakazi, wahitimu, wanafunzi wanaoendelea na wadau wengine.
Akikabidhi msaada huo jana katika kituo hicho, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Vincent Mpepo aliwapongeza walezi hao kwa kazi nzuri ya huduma kwa watoto hao na kuwaomba waendelee na moyo huo kwani wanafanya kitu chema machoni pa wanadamu na Mungu.
Alisema binafsi aliguswa baada ya kuona picha za mnato na mjongeo zilizosambazwa na Inspekta Dominic Msangi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, aliyekuwa Polisi Kata wa Kijiji cha Magagura, Songea Vijijini ambaye alikuwa akiwasihi na kuwaomba wadau na taasisi mblimbali kutembelea katika Kituo hicho ili kuwafariji watoto hao kwa kile watakachojaaliwa.
Huu ni mwanzo tu, mimi kama mwakilishi wa chuo na wadau mbalimbali tutaongeza juhudi kuwatembelea na kusaidia kadiri tutakavyojaaliwa, alisema Mpepo.
Aidha alitoa wito kwa jamii kuungana na kusaidia wahitaji popote walipo badala ya kuwaachia walezi wa vituo pekee hilo na kulishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana nao katika kufanikisha zoezi hilo.
Pamoja na msaada huo, amehaidi kwa kushirikiana na uongozi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania kufadhili upatikanaji wa bima za afya kwa watoto 50 ambazo zitasaidia katika matibabu kwa Watoto hao kutakapokuwa na changamoto ya kiafya.
Kwa upande wake, Inspekta Dominic Msangi alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Kamishna wa Polisi Jamii unaolenga kushirikiana na wadau mbalimbali katika kurudisha fadhila kwa jamii.
“Jeshi la Polisi linashirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo za elimu ili kuchochea mshikamano wa kijamii na kusaidia makundi yenye uhitaji maalum, ikiwemo watoto wanaolelewa katika vituo kama Chipole”, alisema Inspekta Msangi.
Akizungumza kwa niaba ya kituo hicho, Mtawa Maria Akwinata O.S.B kutoka Shirika la Watawa wa Chipole alisema kituo hicho kinahudumia watoto wa rika mbalimbali hata wanaozaliwa siku hiyo hadi wanapofikia shule za sekondari.
Sanjali na hilo, aliushukuru uongozi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania kwa mchango wao walioutoa kituoni hapo na kueleza kuwa kazi ya kulea watoto hao ni kubwa na inahitaji msaada endelevu ili kuweza kukidhi mahitaji ya watoto hao.
Naye Richard Haule, aliyewakilisha watoto wa kituo hicho, ameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu Huria na Jeshi la Polisi kwa msaada huo, akisema kuwa wamefarijika sana na kuona kuwa jamii haijawasahau.
Aidha, aliwaomba wadau wengine ikiwemo taasisi binafsi na za umma kuendelea kujitokeza kusaidia watoto hao ili kuwajengea matumaini na maisha bora ya baadaye.




No comments