Header Ads

DOTK-BAR

MAKAMU WA RAIS MPANGO AONGOZA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI WA SADC NCHINI MADAGASCAR





Na Mwandishi Maalum, Antananarivo – Madagascar

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ Troika Summit) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Ivato, Antananarivo – Madagascar.

Mafanikio ya Tanzania katika Uenyekiti wa SADC-Organ

Akifungua mkutano huo, Dkt. Mpango alisema Tanzania, kupitia uenyekiti wake wa mwaka mmoja uliopita, imefanikisha hatua kubwa katika uimarishaji wa demokrasia, usalama na utawala bora ndani ya kanda. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na:

Kuunda na kuongoza misheni nne za waangalizi wa uchaguzi katika nchi wanachama; Msumbiji, Botswana, Mauritius na Namibia, ambazo zote zilifanyika kwa amani na kuzingatia kanuni za kidemokrasia za SADC.

Kuunganisha michakato ya Luanda Peace Process na Nairobi Peace Process kuhusu mgogoro wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa mara ya kwanza chini ya mwamvuli wa ushirikiano wa SADC na EAC.

Kuweka msisitizo katika mapambano dhidi ya ugaidi, uhamiaji haramu na migogoro ya ndani inayotishia ustawi wa kanda.

Ushirikiano wa Kikanda na Changamoto za Usalama

Makamu wa Rais alisisitiza umuhimu wa Afrika kutumia mbinu na rasilimali zake kukabiliana na changamoto za usalama, akibainisha kauli ya “Suluhu za Kiafrika kwa matatizo ya Afrika.”

Amesema licha ya hatua zilizopigwa, SADC bado inakabiliwa na changamoto kama ugaidi, uhamiaji haramu, ufisadi na usambazaji haramu wa silaha, hivyo inahitajika mshikamano wa pamoja kwa ajili ya kulinda amani na mshikamano wa kikanda.

Uchaguzi Mkuu wa Tanzania Oktoba 2025

Katika hotuba yake, Dkt. Mpango pia aliufahamisha mkutano huo kuwa Tanzania imepanga kufanya Uchaguzi Mkuu wake tarehe 29 Oktoba 2025. Ameeleza kuwa maandalizi muhimu yamekamilika kupitia Tume Huru ya Uchaguzi, na kwamba uchaguzi huo utakuwa wa amani na wa kuaminika. 

Aidha, amealika waangalizi wa uchaguzi wa SADC kushiriki katika mchakato huo.

Pongezi kwa Uongozi wa Rais Samia

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Thabit Kombo, alisema Tanzania imepokea pongezi nyingi kutokana na uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika SADC Organ Troika. Mafanikio yaliyotajwa ni pamoja na:

Kuandaa kikao cha pamoja cha kwanza kati ya SADC na EAC kuhusu amani ya Mashariki mwa DRC.

Kuwezesha vikao vya mara kwa mara vya Wakuu wa Nchi wa SADC Organ Troika.


Kushughulikia migogoro ya Lesotho, Eswatini, jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji, pamoja na migogoro midogo ya mipaka.

Uenyekiti Kukabidhiwa Malawi

Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), utakaofanyika tarehe 17 Agosti 2025, utashuhudia Tanzania ikikabidhi rasmi uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC-Organ kwa Jamhuri ya Malawi

✍🏽 Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, 16 Agosti 2025 – Antananarivo, Madagascar

No comments

Powered by Blogger.