Header Ads

DOTK-BAR

MADINI CHUNYA KUPATA NGUVU MPYA: DC AELEZA MIKAKATI KABAMBE




📍Chunya, Songwe


Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbarak Alhaji Batenga, ameweka wazi mikakati kabambe ya kuimarisha sekta ya madini wilayani humo, ikiwemo ujenzi wa kituo kipya cha kuzalisha umeme (Substation) chenye uwezo wa kuzalisha megawati 90, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wachimbaji na wawekezaji katika wilaya hiyo na maeneo jirani.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Madini Diary Oktoba 9, 2025, Mhe. Batenga alisema kituo hicho kitajengwa eneo la Makongorosi – Chunya, na kitahudumia Chunya na Mkoa wa Songwe. Alitaja miradi inayotarajiwa kunufaika na kituo hicho kuwa ni pamoja na Mgodi wa Shanta–New Luika, Mtambo wa Uchenjuaji wa Anglo De Beers, na Mgodi wa Porcupine North.

 “Kwa sasa tunatumia megawati 9 pekee huku mahitaji halisi yakiwa megawati 90. Kupitia kituo hiki, tutaanza kuzalisha megawati 45 za awali ili kuchochea uchimbaji wa kisasa kwa gharama nafuu,” alisema Batenga.


Ameongeza kuwa mahitaji ya umeme kwenye shughuli za uchimbaji ni makubwa, hivyo ametoa wito kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuweka kipaumbele katika kusambaza umeme kwenye maeneo yenye shughuli za madini, jambo litakalopunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija katika sekta hiyo.

Aidha, DC Batenga amegusia ujio wa kampuni kubwa ya kimataifa ya uchimbaji madini – Anglo De Beers, yenye leseni katika Wilaya ya Chunya, huku tayari ikiwa imeanza kazi eneo la Mbangala mkoani Songwe.

Akimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya madini, Batenga alisema zaidi ya leseni 1,500 zimelenga kuwanufaisha wachimbaji wadogo Chunya, akitoa wito wa kuendelea kutoa leseni ambazo hazijaendelezwa ili wachimbaji wenye nia ya dhati wapate nafasi ya kuziendeleza.

Katika hatua nyingine, ameiomba Wizara ya Madini kufanya tafiti zaidi kubaini maeneo mapya yenye madini ili kuwawezesha wachimbaji kuepuka uchimbaji wa kubahatisha. Ameshauri pia kupatikana mitambo nafuu ya uchorongaji miamba ili kuwezesha wachimbaji wadogo kumudu gharama za utafiti.

“Sisi Chunya hatuchimbi dhahabu pekee. Kwa sasa kuna kiwanda cha kuchenjua shaba, hivyo wachimbaji waanze pia kuangalia fursa za madini hayo,” alisisitiza Batenga.



Akizungumzia taswira ya kiuchumi ya wilaya hiyo, Batenga alisema tarafa mbili za Kiwanja na Kipambawe zina utofauti wa kipekee – Kiwanja ni maarufu kwa madini, huku Kipambawe ikiongoza kwa kilimo cha tumbaku.

Kwa sasa, alisema, sekta za madini na tumbaku zinachangia asilimia 60 ya fedha za maendeleo kwenye mfuko mkuu wa serikali, ikilinganishwa na asilimia 40 ya miaka ya nyuma.

 “Ndani ya miaka mitano ijayo, tunatarajia Chunya kuchangia hadi asilimia 80 kutokana na mapato ya madini na tumbaku. Kwa sasa Halmashauri inanufaika na zaidi ya shilingi bilioni 5 kutoka sekta hizo mbili,” alibainisha.


#Vision2030: Madini ni Maisha na Utajiri

#MadiniDiary #Chunya #Songwe #Uwekezaji #SamiaSuluhu #CentralTV

No comments

Powered by Blogger.