Bar Zimegeuka Maficho ya Upweke: Hadithi Isiyosemwa ya Mapenzi ya Siri
Na Dotto Kwilasa – JICHO LA TATU
Katika giza jepesi la mwanga wa taa za baa, nyuma ya glasi za bia na tabasamu la haraka, kuna simulizi zenye uzito. Simulizi za wanaume waliooa wanaotafuta faraja, na wanawake wanaouza siyo tu pombe, bali pia usikivu unaouzwa kwa bei ya hisia.
Hii si hadithi ya kulaani. Bali ni ya kuangalia upande mwingine wa maisha ya mijini pale penye kelele za muziki lakini kimya cha ndani kinalia,Pale ambapo wanaume wanapoteza mwelekeo wa ndoa, na wanawake wanajikuta katika mahusiano yasiyo rasmi kwa sababu ya hali ngumu za maisha.
Wanaume wengi huingia kwenye baa wakitaka kujiondoa kwenye presha ya maisha huku Wengine hawapokelewi nyumbani kwa heshima, na baa huwapa hifadhi ya muda.
Huko wanaitwa “boss”, na majina mengine ya mahaba wanahudumiwa kwa tabasamu, na ghafla wanahisi thamani yao ipo juu.
Ndipo hapo uhusiano wa 'kijanja’ huanza. Mhudumu wa baa anaweza asiwe na nia mbaya, lakini akakuta anatamani mtu anayemsikiliza zaidi ya mteja mwingine. Mteja naye anatamani zaidi ya bia anataka mtu anayemsikiliza bila kumkosoa.
Hivyo mahusiano ya siri huanza. Si rasmi, si salama, lakini ni halisi.
Kwa wengine, ni uhusiano wa kiuchumi mhudumu anapata msaada wa pesa, mwanaume anapata “faraja” na kutoroka majukumu. Kwa wengine ni zaidi ya hivyo wanaangukia mapenzi ya kweli kwenye mazingira yasiyokuwa ya kawaida.
Lakini mapenzi haya mara nyingi ni ya kuumiza kwa sababu Wake nyumbani wanalia kimya kimya hawapati huduma stahiki pesa yote inapelekwa Bar.
Jamii yetu ina desturi ya kulaani matokeo badala ya kuangalia chanzo. Tunawalaumu "wanaoiba waume za watu", lakini hatuulizi kwa nini waume wanajiachilia kuibiwa.
Tunawashangaa wanaume walioanguka, lakini hatuulizi walikuwa wakikimbia nini.
Ni kweli wapo wanaume dhaifu, wanaotaka kila kitu bila kujituma. Wapo pia wanawake waliogeuza bar kuwa jukwaa la maamuzi ya moyo. Lakini wapo pia waliokwama kwenye ugumu wa maisha na upweke usioonekana.
Wanaume wanahitaji kurudi kwenye misingi ya ndoa zao na Wanawake wa baa wanahitaji nafasi ya kujituma kupata mbadala wa kuishi bila kutegemea mihemko ya wateja wao. Na jamii nzima inahitaji kuacha kufumbia macho mzizi wa tatizo.
Kuna wingi wa waliokata tamaa, waliodanganywa, na wanaotafuta upendo hata kwenye sehemu isiyofaa.
Tumezoea kusema “wanaiba waume za watu,” lakini tumesahau kuwa baadhi ya waume waliamua kuibiwa. Na baadhi ya wahudumu wa baa waliamua kukubali si kwa tamaa, bali kwa kuwa hawakuwa na njia nyingine ya kupendwa, kusaidiwa, au kueleweka.
Jicho la tatu linatuambia kuwa Mapenzi hayawezi kutengenezwa kwenye chupa ya bia.


No comments