Header Ads

DOTK-BAR

POLEPOLE AJIUZULU NAFASI YA UBALOZI NCHINI CUBA




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, ametangaza kujiuzulu rasmi nafasi yake hiyo ya kidiplomasia baada ya kuwasilisha barua kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiomba kuachia nafasi hiyo aliyokabidhiwa na Serikali.

Kupitia taarifa aliyoweka kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Balozi Polepole amesema amefanya uamuzi huo kwa hiari baada ya kutafakari kwa kina huku akibainisha kuwa hatua hiyo imefuata taratibu zote rasmi za kibalozi.

 "Nimemwandikia Mheshimiwa Rais barua ya kuomba kuachia nafasi ya uwakilishi wangu kama Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba," ameandika Polepole.


Balozi huyo ambaye pia aliwahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuteuliwa, aliteuliwa katika nafasi hiyo ya ubalozi mwezi Juni mwaka 2023 na kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Serikali ya Cuba muda mfupi baada ya uteuzi wake.

Katika kipindi cha uwakilishi wake, Polepole alihusika moja kwa moja katika kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Cuba katika maeneo ya afya, elimu, na uhusiano wa kidiplomasia, huku akihimiza mabadilishano ya maarifa na teknolojia kati ya nchi hizo mbili.

Polepole ametoa sababu mahususi za uamuzi wake huo kuwa ni kutoridhishwa na uongozi uliopo madarakani .

Licha ya hayo amesisitiza kuwa ataendelea kuwa mzalendo na mtumishi wa Taifa katika maeneo mengine yoyote atakayopangiwa majukumu.

Taarifa hiyo imezua mijadala mingi mitandaoni, huku baadhi ya wadau wa masuala ya diplomasia wakitafsiri hatua hiyo kama sehemu ya mabadiliko ya kawaida ndani ya utumishi wa umma, hasa katika nafasi nyeti kama za mabalozi.

Serikali bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu mrithi wa nafasi hiyo, lakini mchakato wa uteuzi wa Balozi mpya unatarajiwa kufanyika kwa mujibu wa taratibu za kidiplomasia.




No comments

Powered by Blogger.