Trilioni 1.5 Zageuza Shinyanga: Serikali Yajenga Maendeleo Yanayoonekana
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeupeleka Mkoa wa Shinyanga kwenye hatua mpya ya maendeleo kupitia uwekezaji mkubwa wa miradi ya kijamii, kiuchumi na kimkakati.
Kwa kipindi cha miaka minne, Mkoa wa Shinyanga umepokea zaidi ya shilingi trilioni 1.563 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, maji, miundombinu, nishati, kilimo, na madini.
Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Mboni Mohamed Mhita, amesema fedha hizo zimechangia kuboresha maisha ya wananchi kwa kuimarisha huduma za msingi kama shule, hospitali, barabara na usambazaji wa umeme.
Katika sekta ya elimu, Mkoa ulipokea shilingi bilioni 155.24 na kujenga shule mpya, mabweni, maktaba, maabara na vyuo. Shule za sekondari zimeongezeka kutoka 186 hadi 200, huku vyumba vya madarasa ya sekondari vikifikia 2,865 kutoka 1,583 mwaka 2020.
Upande wa afya, shilingi bilioni 79.1 zilitumika kujenga na kukarabati hospitali, vituo vya afya, zahanati na nyumba za watumishi. Hospitali za wilaya zimeongezeka kutoka 2 hadi 7, huku watumishi wa afya wakiongezeka hadi kufikia 2,812.
Maji nayo yamepewa kipaumbele, ambapo shilingi bilioni 113.33 zilitumika kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi. Vijiji vyenye huduma ya maji vimeongezeka kutoka 162 hadi 384 na miradi mikubwa kama ule wa Ziwa Victoria inaendelea kutekelezwa.
Katika sekta ya mapato, Mkoa umeongeza ukusanyaji kutoka bilioni 199 hadi bilioni 202.54, sawa na asilimia 102 ya lengo. Vyanzo vya mapato vimeboreshwa kupitia mirabaha, leseni, CSR na ushuru wa mazao na mifugo.
Mafanikio katika sekta ya madini nayo ni ya kihistoria. Mkoa umekusanya zaidi ya bilioni 540 kutokana na shughuli za madini, huku wachimbaji wadogo waliopewa leseni wakiongezeka kutoka 332 hadi 1,766. Fedha za madini zimechangia miradi mingi ya maendeleo.
Mhe. Mhita amesema mafanikio haya yamewezekana kwa sababu ya uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia na ushirikiano wa wananchi. Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wote kuhakikisha maendeleo haya yanakuwa endelevu.




No comments