Bilioni 41 Zaiinua Afya Katavi, Huduma Za Kibingwa Zapatikana Ndani ya Mkoa
Na Dotto Kwilasa, Katavi
Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuleta mageuzi katika sekta ya afya mkoani Katavi kwa kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 41 katika kipindi cha miaka mitano kwa ajili ya kuboresha huduma na miundombinu ya afya katika maeneo yote ya mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amesema fedha hizo zimetumika kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, hospitali nne za wilaya, vituo vya afya 11, zahanati 47, pamoja na ukarabati wa hospitali ya zamani ya Manispaa ya Mpanda.
Ameeleza kuwa idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kutoka 102 mwaka 2021 hadi 161 mwaka 2025, ongezeko la asilimia 36.64 ambalo limepunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma bora.
Zahanati zimeongezeka kutoka 80 hadi 127, na vituo vya afya kutoka 17 hadi 28, hatua iliyosaidia pia kupunguza msongamano katika hospitali za wilaya na kuongeza upatikanaji wa huduma katika maeneo ya vijijini.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa imepokea zaidi ya shilingi bilioni 18 kwa ajili ya kukamilisha majengo muhimu, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa kama CT-Scan, digital X-Ray na mashine za dialysis, na sasa inatoa huduma za kibingwa kwa mara ya kwanza ndani ya mkoa.
Aidha, bajeti ya dawa imeongezeka kwa asilimia 11.8 kutoka shilingi bilioni 2.98 mwaka 2021 hadi 3.38 mwaka 2024, huku wastani wa upatikanaji wa dawa ukifikia asilimia 94 kufikia Juni 2025.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema pia vituo vya huduma za dharura kwa wajawazito (CEmONC) vimeongezeka kutoka 8 hadi 14, huku idadi ya akina mama wanaojifungulia kwenye vituo vya afya ikiongezeka hadi zaidi ya 48,000 kwa mwaka.
Magari ya wagonjwa (ambulance) yameongezeka kutoka 10 hadi 17 ndani ya miaka mitano, jambo ambalo limeongeza ufanisi katika kutoa huduma za rufaa kutoka ngazi ya zahanati hadi hospitali za wilaya na ya rufaa ya mkoa.




No comments