Uwekezaji wa Kaboni Waanza Kuleta Matunda Katavi
Na Dotto Kwilasa, Katavi
Biashara ya hewa ukaa (kaboni) imeanza kuzaa matunda katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, ikiwa ni matokeo ya ushiriki wa jamii katika uhifadhi wa misitu kupitia miradi ya kaboni inayoratibiwa kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amesema utekelezaji wa mradi huo umeleta manufaa ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa vijiji vinavyoshiriki katika hifadhi ya misitu, huku wakipokea mgao wa fedha zinazotokana na kuuza kaboni kwa masoko ya kimataifa.
Amesema kuwa hadi sasa zaidi ya vijiji 17 vimenufaika na mgao wa fedha kutoka katika mauzo ya kaboni, fedha ambazo zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa shule, zahanati, na huduma za maji safi na salama.
“Wananchi wanaelewa kuwa kulinda misitu ni zaidi ya kutunza mazingira. Sasa wanapata kipato halali kutokana na hewa safi wanayosaidia kuhifadhi kupitia miti yao,” alisema Mrindoko.
Mradi wa kaboni pia umesaidia kupunguza shughuli za ukataji miti hovyo kwa ajili ya kuni na mkaa, huku jamii zikihamasishwa kutumia nishati safi na rafiki kwa mazingira kama majiko banifu.
Kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira, misitu ya Katavi inatoa mchango mkubwa katika kuhifadhi hewa ukaa duniani, hivyo kuvutia wawekezaji wa kimataifa wanaotafuta fidia ya uzalishaji wa kaboni katika nchi zao.
Mradi huo unatekelezwa kwa misingi ya ushirikishwaji wa jamii, ambapo vijiji vinakuwa na mamlaka ya moja kwa moja katika kusimamia mapato na kuamua namna bora ya kuyatumia kwa maendeleo ya wananchi.
Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa halmashauri nyingine kuiga mfano wa Tanganyika kwa kubuni njia endelevu za uhifadhi wa mazingira zinazotoa tija kwa wananchi na kulinda urithi wa vizazi vijavyo.


No comments