EGA YAENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA SERIKALI KUPITIA MAGEUZI YA KIDIGITALI SABASABA 2025
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imeendelea kuonesha juhudi za Serikali katika kuleta mageuzi ya kidigitali kupitia Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja Mawasiliano wa eGA, Bi. Subira Kaswaga, alieleza kuwa mamlaka hiyo imepewa jukumu kisheria la kusimamia matumizi ya TEHAMA serikalini kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa umma.
“Katika kutekeleza jukumu hilo, tumeweza kubuni na kuendesha mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayorahisisha kazi za kila siku ndani ya Serikali, huku pia ikitoa fursa kwa wananchi kupata huduma kwa njia za kidigitali kwa urahisi na ufanisi,” alisema Kaswaga.
Miongoni mwa mifumo hiyo ni e-Mrejesho, jukwaa la kidigitali linalowawezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Serikali kwa kutoa maoni, pongezi au malalamiko, ambapo Serikali nayo hutoa mrejesho wa hatua zilizochukuliwa.
Kaswaga alibainisha kuwa mfumo huo unapatikana kwa njia tatu, ikiwemo kupitia simu ya mkononi, na unamruhusu mwananchi kuficha taarifa zake za utambulisho ikiwa hataki kujulikana, huku pia akipatiwa namba ya ufuatiliaji ya taarifa aliyoitoa.
“Kwa mfumo huu, taasisi za umma huweza kutambua maeneo yenye malalamiko ya mara kwa mara, hivyo kuwasaidia viongozi kuchukua hatua stahiki kwa haraka zaidi. Pia mfumo huu huchochea uwajibikaji kwa kuwa viongozi wakuu wa Serikali wanaweza kuona kwa uwazi hatua zinazochukuliwa kwenye kila malalamiko,” aliongeza.
Aidha, alifafanua kuwa mfumo wa e-Mrejesho umeendelea kuleta sifa kwa Tanzania kimataifa, ambapo Julai 7, 2025, ulitangazwa mshindi katika Tuzo za Dunia za Jumuiya ya TEHAMA (WSIS 2025) kwenye kipengele cha Serikali Mtandao.
“Ni fahari kubwa kwa taifa letu kuona mfumo uliobuniwa na Watanzania ukitambulika kimataifa. Tunawahamasisha wananchi kuutumia mfumo huu ili kuimarisha mawasiliano na Serikali na kuongeza ufanisi katika kuhudumiwa,” alisisitiza.
Alihitimisha kwa kutoa wito kwa watumishi wa umma kuzingatia wajibu wao kwa kushughulikia kikamilifu maoni na malalamiko yanayowasilishwa kupitia mfumo huo, ili kujenga imani ya wananchi kwa Serikali na kukuza uwajibikaji wa kitaasisi.


No comments