Header Ads

DOTK-BAR

MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII YATAKIWA KUIMARISHA UWEKEZAJI WA MIUNDOMBINU KWA KUZINGATIA USALAMA WA MICHANGO YA WANACHAMA – DKT. MPANGO




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Arusha, 10 Julai 2025


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa licha ya umuhimu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Barani Afrika kuwekeza katika miradi ya miundombinu, ni lazima kuhakikisha michango ya wanachama inabaki salama na kutosha kwa ajili ya kutimiza malengo yake ya msingi, ambayo ni kuwalinda wanachama dhidi ya misukosuko ya kiuchumi, kijamii na kusaidia kupambana na umaskini.

Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo leo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 14 wa Kimataifa wa Watunga Sera wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Barani Afrika unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika miradi ya miundombinu ni jambo jema lakini unapaswa kufanywa kwa umakini mkubwa, kwani kushindwa kwa miradi hiyo kutekelezeka kunaweza kudhoofisha uwezo wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa wanachama.

Makamu wa Rais ameonya dhidi ya miradi yenye ubunifu usio makini, gharama kubwa kupita kiasi, au ile isiyotekelezeka kwa urahisi, akisema miradi ya namna hiyo huleta hatari ya kuchelewesha au kushindwa kabisa kulipa mafao ya wanachama kutokana na ukosefu wa fedha.

Aidha, Dkt. Mpango amewataka wataalamu wanaoshiriki mkutano huo kuandaa mikakati thabiti itakayowezesha Mifuko bora ya Hifadhi ya Jamii kuwa kichocheo cha ufadhili wa miundombinu ya kijamii na kiuchumi katika maeneo ya vijijini. Amesema maendeleo ya miundombinu vijijini yataongeza tija, kuimarisha ustawi wa wananchi, kupunguza uhamaji wa watu kwenda mijini na kuongeza ajira.

Katika hotuba yake, amebainisha kuwa Afrika inakabiliwa na pengo la kati ya dola bilioni 68 hadi 108 kila mwaka kwa ajili ya ufadhili wa miundombinu, hali inayotoa fursa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwa chombo muhimu katika kuziba pengo hilo na kuchochea maendeleo ya bara hilo.

Dkt. Mpango amewahimiza Watunga Sera wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika kutoa mawazo ya vitendo kuhusu namna bora ya kuhakikisha mifuko hiyo inafanya uwekezaji wenye tija, salama na endelevu katika miradi ya miundombinu.

Mkutano huo umewakutanisha Viongozi wa Afrika wakiwemo Mawaziri, Watunga Sera na Wataalamu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoka mataifa mbalimbali.

Kauli mbiu ya mkutano huo ni: “Mifuko ya Hifadhi ya Jamii: Chachu ya Maendeleo ya Miundombinu na Ukuaji wa Kiuchumi na Kijamii Barani Afrika.”

No comments

Powered by Blogger.