Header Ads

DOTK-BAR

MLUYA WA DP AAHIDI KUONDOSHA ADA YA KUHIFADHI MAITI, KIKOKOTOO NA MAGEUZI MAGEREZANI




Na Dotto Kwilasa, Dodoma


Mgombea urais wa Chama cha Democratic Party (DP), Abdul Juma Mluya, leo Agosti 13, 2025, amechukua rasmi fomu ya kugombea urais katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma, akiambatana na mgombea mwenza wake, Sadous Abrahaman Khatib.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu, Mluya alisisitiza dhamira yake ya kuondoa ada za kuhifadhi maiti, akieleza kuwa gharama hizo zinabeba mzigo usiofaa kwa familia ambazo tayari zimewalipa kodi.

“Hakuna sababu ya familia kulia mara mbili au kuathirika kifedha wakati wa msiba,” alisema Mluya.

Mbali na hilo, Mluya alisisitiza marekebisho makubwa ya mfumo wa kikokotoo cha mafao ya wastaafu. Alieleza kuwa mfumo wa sasa umekuwa chanzo cha kero na dhuluma kwa watumishi waliolitumikia taifa kwa uaminifu.

Kikokotoo kipya kitahakikisha wastaafu wanapata haki zao kikamilifu, kuondoa umaskini, na kujenga misingi imara ya ajira bora.

Aidha, marekebisho hayo yataenda sambamba na mpango wa waajiri kuwapatia wafanyakazi nyumba bora, kupunguza rushwa na kuongeza ari ya kazi.

Mgombea huyo pia alieleza kipaumbele chake cha askari magereza, akisema hali ya sasa ni ngumu kuwatofautisha na wafungwa kutokana na changamoto za kimaisha na mazingira duni ya kazi.

“Tutaboresha maslahi, mafunzo na mazingira ya kazi ya askari magereza ili kurejesha heshima, nidhamu na weledi wa kitaaluma,” alisema.


No comments

Powered by Blogger.