Serikali Yazindua Fursa Mpya kwa Wakulima wa Mwani Tanga
Na Mwandishi Wetu – Tanga
Serikali imewataka wakulima wa mwani nchini kutumia mbinu za kisasa za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. James Kilabuko, wakati wa kufunga mafunzo ya siku 12 yaliyoandaliwa kwa vikundi vya wakulima wa mwani katika Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga, kuanzia tarehe 4 hadi 15 Agosti, 2025.
“Mafunzo mliyojifunza ya kilimo bora cha mwani yatawasaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji na ubora wa mwani katika soko la ndani na nje ya nchi,” alisema Dkt. Kilabuko. Aliongeza kuwa mafunzo ya uongezaji thamani, matumizi salama ya kemikali, ufungaji wa bidhaa, na upatikanaji wa masoko yatawasaidia wakulima kuzitangaza bidhaa zao kwa wateja zaidi.
Dkt. Kilabuko pia alisisitiza umuhimu wa kueneza maarifa yaliyojifunzwa kwa vikundi vingine ambavyo havikupata fursa ya mafunzo, hususan katika masuala ya wokozi na huduma za kwanza majini, akiongeza kuwa elimu ya usalama shambani ni muhimu kuokoa maisha ya wakulima na wenzao.
“Kile mlichojifunza muwafikishie wenzenu ili kuwa na uwelewa wa pamoja katika kuboresha maslahi ya vikundi vyenu,” alisema.
Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Selestine Masalamado, aliwafafanulia washiriki kuwa mafunzo haya ni awamu ya pili ya utekelezaji wa mwongozo wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika bahari na maziwa makuu, uliozinduliwa Februari 2023 na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa.
Awamu ya kwanza ilitekelezwa katika Wilaya za Mafia, Pangani na Bagamoyo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vichanja vya kukaushia dagaa na ununuzi wa boti ya kisasa kwa ajili ya doria baharini.
Kutokana na mafanikio ya awamu ya kwanza, Serikali ya Japan na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) waliendelea kutoa msaada wa kifedha na vifaa, ikiwemo boti mbili za doria, mashine za kusaga mwani, na mafunzo ya uelekezi kwa vikundi 26 vya wakulima wa mwani.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Bw. Rashid Karim Gembe, alipongeza uwepo wa mafunzo na kuahidi kushirikiana na wakulima kuhakikisha malengo ya kiuchumi kupitia zao la mwani yanafikiwa.
Naye Mwakilishi wa UNDP, Bw. Saimon Nkonoki, alisema mafunzo haya yametambulika vyema na yakapokelewa kwa ushirikiano mkubwa, akiahidi kuendeleza msaada na ushirikiano kwa vikundi vyote vilivyonufaika.
Washiriki wa mafunzo walishukuru kwa fursa waliyopewa na kueleza jinsi maarifa mapya yatakavyowawezesha kuboresha mbinu za kifedha, masoko, na utengenezaji wa bidhaa kutoka mwani, ikiwemo sabuni, dawa mbalimbali, na bidhaa nyingine nyingi. Bi. Aisha Jumbe, akiongea kwa niaba ya washiriki, alisema:
“Tunathamini mafunzo haya, kwani yatatupa mbinu mpya za huduma za kifedha, kuandaa bidhaa, na kufikia matokeo bora kutoka shambani hadi sokoni.”
Mafunzo haya yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa kushirikiana na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, kwa ufadhili wa Serikali ya Japan na UNDP, yakilenga kuongeza ujuzi, usimamizi wa vikundi, mnyororo wa thamani, na masoko ya mwani kwa wakulima wa Wilaya ya Mkinga.







No comments