Header Ads

DOTK-BAR

Mpina Aanika Dira ya Urais, Aanzia Mizizi Yake Mwandoya – Simiyu

 

Na Evance Yerico, Dodoma

Mgombea Urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, amezindua rasmi safari yake ya kuwania nafasi ya juu kabisa ya uongozi nchini kwa kuchukua fomu ya kugombea urais katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) leo Agosti 15, 2025, jijini Dodoma.


Akifuatana na mgombea mwenza wake, Fatma Abdulhabib Fejej, Mpina ametangaza kuanza harakati za kusaka wadhamini katika Mwandoya, kijiji kilichopo Jimbo la Kisesa mkoani Simiyu, ambako alizaliwa na kukulia.


Amesema uamuzi wa kuanzia nyumbani una maana ya kipekee kwake, kwani ni ishara ya kurudi kwenye mizizi na kuomba ridhaa ya jamii iliyoshuhudia mwanzo wa safari yake ya maisha.

“Nilipozaliwa ndipo ninapoanza kutafuta dhamana ya kuongoza taifa hili. Ni jambo la heshima na shukrani kwa jamii yangu,” alisema Mpina mbele ya waandishi wa habari.

Mpina ametoa mwito kwa wananchi, hususan vijana, kujitokeza kwa wingi kuunga mkono mchakato wa kidemokrasia kwa kumdhamini yeye na chama chake, akisisitiza kuwa huu si wakati wa kufuata siasa za vyama pekee bali kutanguliza maslahi ya taifa.

“Niwaombe vijana wajitokeze kwa wingi ili tupate sifa. Hawatafuata mambo ya vyama bali watasimamia maslahi ya taifa,” aliongeza.

Mchakato wa kukusanya wadhamini utaendelea katika mikoa mingine baada ya Simiyu, huku vipaumbele vya ACT Wazalendo vikitarajiwa kutangazwa rasmi pindi zoezi hilo litakapokamilika.









No comments

Powered by Blogger.